- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Wanawake wa Sumatra: Sio Tu Wahanga wa Mafuriko
(Imetafsiriwa)
Habari:
Maafa ya mafuriko katika kisiwa cha Sumatra yamesababisha vifo vya watu 1,071 kufikia 19 Disemba kulingana na Abdul Muhari, Mkuu wa Kituo cha Data, Taarifa, na Mawasiliano ya Maafa katika Shirika la Kitaifa la Usimamizi wa Majanga la Indonesia (BNPB). Katika majanga, wanawake na watoto mara nyingi huwa waathiriwa mara mbili kutokana na udhaifu wa kimuundo, ikiwemo kupuuzwa kwa mahitaji ya afya ya uzazi ya wanawake. Taasisi ya Msaada wa Kisheria ya Banda Aceh (LBH) imesisitiza kwamba katika kila janga, wanawake ndio kundi linaloathiriwa zaidi lakini lisiloonekana sana—mpangilio ambao umethibitishwa tena katika mgogoro wa sasa. Katikati ya juhudi za kukabiliana na dharura, LBH ilisaidia kesi ya unyanyasaji wa kijinsia unaomhusisha mwanafunzi mmoja wa kike anayetafuta makaazi, ikisisitiza jinsi dhulma ya kijinsia inavyoongezeka wakati hali za dharura.
Zaidi ya kuwa waathiriwa wa mafuriko, wanawake wa Sumatra pia wananyonywa na ulafi wa ubepari, haswa ndani ya tasnia kubwa ya mafuta ya mawese. Kufikia Julai 2025, takriban wafanyikazi milioni 16.2 wameajiriwa katika sekta ya mafuta ya mawese ya Indonesia, huku wanawake wakichangia katika silsila yote ya usambazaji—kutoka shughuli za juu hadi chini. Kwa zaidi ya miongo mitatu, takriban wanawake milioni 4.9 wamefanya kazi kama vibarua vya kila siku (BHL), wakifanya kazi ngumu za kimwili kama vile kuweka mbolea, kunyunyizia dawa za kuua wadudu, kupanda, na kupalilia. Kazi hizi huwaweka katika hatari kubwa za kiafya na usalama, pamoja na tishio la unyanyasaji wa kijinsia, hasa kutokana na maumbile ya mashamba hayo ya mafuta ya mawese yaliyojificha na yaliyo sehemu za kando.
Sekta ya mafuta ya mawese ndiyo chanzo kikuu cha ukataji miti huko Sumatra, huku upotevu wa misitu ukitarajiwa kuzidi hekta milioni 7 ifikapo mwaka wa 2026. Uharibifu huu wa mazingira sio tu kwamba huongeza hatari za maafa ya hali ya hewa lakini pia husababisha mgogoro mkubwa wa kijamii kwa kuwanyonya mamilioni ya wanawake. Uchambuzi uliofanywa na Timu ya Uandishi wa Habari za Data ya Kompas uligundua kuwa katika kipindi cha miaka 34 iliyopita, misitu huko Aceh, Sumatra Kaskazini, na Sumatra Magharibi imepungua kwa hekta milioni 1.2—karibu hekta 100 zinapotea kila siku kwa miongo mitatu. Katika kipindi hiki hiki, mamilioni ya wanawake wa Sumatra wamebeba gharama ya uharibifu huu kupitia unyonywaji katika tasnia ya mafuta ya mawese.
Maoni:
Kumekuwa na maonyo mengi kuhusu hatari mbili za simulizi yenye sumu ya “uwezeshaji wa wanawake ya kibepari,” ambayo hatimaye hutumikia maslahi ya kipote cha ubepari. Mafuriko ya Sumatra mwanzoni mwa Disemba 2025 yalifichua zaidi kwa ulimwengu kwamba wanawake wa Sumatra ni waathiriwa maradufu wa unyonyaji wa kibepari wa viwanda, kwa muda mfupi pamoja na muda mrefu.
Sumatra imekuwa eneo muhimu la ubepari wa mipakani—mpaka mpya ambapo ubepari unapanuka ili kukusanya faida kwa kuchimba maliasili, kuuza na kunyonya nguvukazi ya wanawake, miili, na nafasi za kijamii, na kubadilisha vipengee vingi vya maisha ya wanawake. Christian Lund, katika Sheria ya Kumi na Tisa, inabainisha Sumatra Kaskazini na Aceh kama mifano ya kawaida ya maeneo ya mipaka ambayo yanaendelea kubadilishwa na upanuzi wa bidhaa za kimataifa, kutoka mashamba makubwa ya enzi za ukoloni na misitu hadi miundombinu ya kisasa ya mafuta ya mawese na nishati. Katika miongo miwili iliyopita, mpaka huu umefikia umbo lake kali zaidi kupitia upanuzi wa haraka wa tasnia ya mafuta ya mawese. Mamilioni ya hekta za misitu zimesafishwa, ardhi za chemichemi zimekaushwa maji, na maeneo muhimu ya vyanzo vya maji yamebadilishwa.
Kwa hivyo, ahadi za ustawi kwa wanawake wa Sumatra—zinazoundwa kwa kuwashajiisha kufanya kazi kama njia ya kupunguza umaskini na uwezeshaji—sio tu za uongo bali pia ni za udanganyifu mkubwa. Simulizi hii ya ustawi ni ya uongo, kwani inaficha ukweli kwamba utumiaji wa mfumo wa kiuchumi wa kibepari wa misitu ya Sumatra wenyewe ndicho chanzo kikuu cha umaskini na upotevu wa kimfumo wa uwezeshaji wa wanawake, ndani ya nchi na kimataifa.
Chini ya mfumo huu na sera zinazouendeleza, mamilioni ya wanawake wa Sumatra wataendelea kuvumilia shida kubwa ya kiuchumi, bila kujali kama wanashiriki katika kazi ya kulipwa au la. Wanabaki kuwa waathiriwa maradufu wa ulafi wa rasilimali. Kama Mwenyezi Mungu Mtukufu asemavyo:
[ظَهَرَ الْفَسَادُ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ بِمَا كَسَبَتْ أَيْدِي النَّاسِ لِيُذِيقَهُم بَعْضَ الَّذِي عَمِلُوا لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ]
“Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu.” [ Ar – Rum: 41].
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Dkt. Fika Komara