Jumatano, 27 Jumada al-thani 1447 | 2025/12/17
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

Afisi ya Habari
Kitengo cha Wanawake

H.  15 Jumada II 1447 Na: H 1447 / 032
M.  Jumamosi, 06 Disemba 2025

Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Chuo Kikuu cha Al-Quds Kinafanya Kongamano kwa Ufadhili wa Magharibi na Programu Iliyoundwa na Magharibi Chini ya Kauli Mbiu “Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake”
(Imetafsiriwa)

Mnamo Jumanne, 2 Disemba 2025, Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Al-Quds – Abu Dis kilizindua kongamano la kimataifa lililopewa kichwa “Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake: Changamoto, Masuluhisho, na Mbinu Bora katika Eneo la Mediterania,” kwa ushirikiano na Wizara ya Masuala ya Wanawake ya Palestina, Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kupambana na Ukatili Dhidi ya Wanawake, Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA), na Chuo Kikuu cha Perugia, Italia, kwa usaidizi wa ushirikiano wa Italia.

Katika siku ya kwanza ya kongamano hilo, watafiti waliwasilisha nyaraka zao, ambazo zilionyeshwa na kujadiliwa katika bewa kuu la Chuo hicho kikuu. Wasomi, wataalamu, watunga sera, na wawakilishi kutoka asasi za kiraia walishiriki katika majadiliano na kusikiliza matokeo, ambayo yalipangwa kwa mada kuu nne: Ukatili dhidi ya wanawake, usawa wa kijinsia katika soko la ajira na mahali pa kazi, wanawake na jamii, na sekta za jinsia na serikali, ikiwa ni pamoja na kuzingatia uzoefu wa Italia. Kongamano hilo lilichukua siku tatu. Siku ya pili ilijumuisha majadiliano ya meza ya duara na washirika wa asasi za kiraia, ambapo utafiti uliotumika uliwasilishwa katika Kituo cha Wanawake cha Mwongozo wa Kisheria na Kijamii. Siku ya mwisho ilitengwa kwa ajili ya warsha iliyofanyika katika Wizara ya Masuala ya Wanawake na mashirika mengine husika ya serikali. Kongamano lilihitimishwa kwa majadiliano ya meza ya duara yaliyowaleta pamoja maafisa wa serikali, washirika, watafiti, na mashirika ya kiraia ili kuunda mpango wa kutekeleza mapendekezo ya mwisho ya kongamano hilo.

Kongamano hili, lililofadhiliwa na kupangwa na Magharibi na kuhudhuriwa na watu wanaoshukiwa na mashirika yanayohusiana na CEDAW, linaingia ndani ya muundo wa vita visivyokoma vinavyoendeshwa na dola za kikoloni za Magharibi na zana zao dhidi ya Uislamu na hukmu zake, hasa zile zinazohusu mfumo wa kijamii, zinazoangazia wanawake na kuibua kaulimbiu za udanganyifu na zisizoeleweka kama vile usawa, uwezeshaji, na haki. Hili linaakisiwa katika kichwa cha kongamano, “Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake,” kaulimbiu zinazoficha sumu ndani ya asali. Kupitia kaulimbiu hizi, zinawahimiza wanawake kuasi dhidi ya hukmu za Mola wao Mlezi na mwongozo wa Mtume Wake (saw), kuacha ulinzi wa familia zao na waume zao, na kuwaasi. Zaidi ya hayo, huwaletea wanawake mateso, wakiwabebesha majukumu zaidi ya uwezo wao, na kuwalazimisha kukiuka maumbile yao ya asili na umbo la kibiolojia ili wawe sawa na wanaume, ambao kimsingi ni tofauti nao katika uwezo na nguvu. Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwaumba wanaume na wanawake na akawapa majukumu kila mmoja kulingana na umbile na uwezo wao. Aliwafanya wawe sawa katika baadhi ya majukumu na hukmu, huku akimpa mmoja pasi na mwengine hukmu na majukumu, bila kupunguza hadhi ya yeyote kati yao. Kwa kisingizio cha kuwawezesha wanawake, wamewageuza kuwa vyombo vya kunadi bidhaa zao, wakiwalazimisha kufanya kazi ili wapate riziki ili wasiwe “chini ya huruma ya wanaume!” Wanawanyonya katika kazi ngumu na kuwalipa mishahara ya chini kabisa. Fikra na kaulimbiu hizi hazina thamani na zingewanufaisha watetezi wao kama zingekuwa na faida yoyote. Fikiria hali ya wanawake katika nchi zinazopigia debe kaulimbiu hizi, ikiwemo Italia, ambayo “uzoefu wake katika uwanja huu” unadaiwa kutumika kama mfano, ambapo mwanamke mmoja huuwawa kila baada ya siku tatu na mwenzi wake au familia yake!

Vyuo vikuu kimsingi vimekusudiwa kuwa mwenge wa elimu na tabia njema, si majukwaa ya ufisadi na fikra chafu. Kusudi lao ni kuzalisha vizazi vilivyoelimika na vyenye ufahamu vinavyojali sana Ummah wao na dini yao na kujitahidi kwa ajili ya maendeleo yake. Basi, tunaweza kusema nini kuhusu vyuo vikuu katika Ardhi Iliyobarikiwa ya Palestina, ambapo watu wa Gaza wanapitia vita vya kikatili vya kuangamizwa, na wale walio katika Ukingo wa Magharibi wanakabiliwa na uhalifu wa jeshi la Mayahudi na magenge ya walowezi, ardhi zao kunyang'anywa, nyumba na mali zao kubomolewa, na maisha yao kufanywa kuwa mabaya mno katika jaribio la kuwalazimisha kuondoka? Sio mbali na chuo kikuu kinachoitwa al-Quds, watu wake wanapitia unyanyasaji na mateso, na Msikiti wa Al-Aqsa unanajisiwa, huku swala na ibada za Talmud zikifanywa ndani ya maeneo yake matakatifu. Kwa hivyo, ni wazi kwamba kulengwa kwa shule na vyuo vikuu na kuzingatia kwao sio bila sababu, bali ni kuzalisha vizazi vilivyotengwa na Dini na Ummah wao, vizazi ambavyo havijali maendeleo yake au ukombozi wa ardhi yake na maeneo yake matakatifu.

Kwa kusisitiza kufanya kongamano hili licha ya kukataliwa na watu wa Palestina na maombi yao ya kufutiliwa mbali, na licha ya maandamano ya wanafunzi, viongozi wa jamii, na wazazi, idara ya chuo kikuu imejifedhehesha na kushiriki katika shughuli hizi za kutiliwa shaka. Imethibitisha kwamba pesa za wafadhili wake zina thamani zaidi kwake kuliko dini na heshima, na kwamba neno lao ndio kuu. Wanaweka masharti na utashi wao badali ya ufadhili huu wa kisiri. Angalia matokeo na mapendekezo ya kongamano hilo, na utaona kwamba miongoni mwa vipengee vyake ni marekebisho au kufutwa kwa sheria zilizopo, hasa sheria za hadhi ya mtu binafsi, kwa mujibu wa CEDAW, ambayo inagongana na Sharia ya Kiislamu na vinatoa wito wa “kubadilisha au kurekebisha sheria” ili kuendana na vipengee vyake. Zaidi ya hayo, ikiwa vyombo vinavyounga mkono na kushiriki katika kongamano hili kweli vinajali kuhusu wanawake wa Palestina, kama wanavyodai, kwa nini hatujasikia hata neno moja kutoka kwao kuhusu uhalifu wa kikatili uliofanywa dhidi ya wanawake hawa na umbile la Kiyahudi? Kwa nini hawajachukua hatua ya kuwanusuru na kupunguza mateso yao? Je, inawezekana kwamba bado kuna watu nchini Palestina ambao bado hawajagundua umbile halisi la vyombo na taasisi hizi na malengo yao maovu?

Kwa kumalizia, tungependa kusisitiza jambo muhimu: Hatupingi wanawake kupokea haki walizopewa na Shariah ya Kiislamu, wala hatupingi wao kuwa na nafasi yao halali na dori yao changamfu katika jamii. Msidanganyike na majaribio ya kupotosha taswira ya Uislamu na kuutuhumu kuwakandamiza wanawake na kuwanyima haki zao. Chunguzeni maandiko ya kidini, maisha ya Waislamu, na historia yao ili kugundua hadhi hii ya juu na haki ambazo Uislamu umewapa wanawake. Wallahi, tunatamani yaliyo kheri na yenye manufaa kwao katika dunia hii na akhera, huku watu hawa mafisadi wakitamani mateso na maangamivu kwao katika maisha yote mawili.

Enyi Watu wa Ardhi Iliyobarikiwa, na Enyi Vijana na Wanawake:

Simameni imara dhidi ya njama zinazopangwa dhidi yenu na familia zenu. Mcheni Mwenyezi Mungu katika mambo ya Dini yenu, heshima yenu, na watoto wenu. Msiwaache wakiwa katika hatari ya kudhulumiwa na dola za kikoloni na vibaraka wao.

[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَاراً وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ]

“Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa anayo waamrisha, na wanatenda wanayo amrishwa.” [At-Tahrim 66:6]

Kitengo cha Wanawake
katika Afisi Kuu ya Habari
ya Hizb ut Tahrir

Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari
Kitengo cha Wanawake
Address & Website
Al-Mazraa Sanduku la Posta. 14-5010 Beirut- Lebanon
Tel: 00961 1 30 75 94 Mobile: 00961 71 72 40 43
www.muslimworld.today
Fax: Telefax
E-Mail: ws-cmo@muslimworld.today

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu