- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Utawala wa Sharaa nchini Syria Haujui Mipaka Katika Kujisalimisha Kwake kwa Marekani
(Imetafsiriwa)
Habari:
Rais wa Marekani Donald Trump alituma barua iliyoandikwa kwa mkono kwa kiongozi wa Syria Ahmed Sharaa, akisisitiza uungaji mkono wake na kuahidi msaada wa Marekani. Barua hiyo iliwasilishwa Damascus kupitia Tom Barrack, mmoja wa washirika wa karibu wa Trump na mfanyibiashara wa kimataifa. Picha ya wakati Trump alipokutana na Sharaa katika Afisi ya Oval iliambatanishwa na barua hiyo. Trump aliandika barua ifuatayo kwenye picha hiyo kwa mwandiko wake mwenyewe: “Ahmed, utakuwa kiongozi mzuri, na Amerika itasaidia!” (Mashirika, 3 Disemba 2025)
Maoni:
Tangu siku alipochukua madaraka, Tom Barrack, Balozi wa Marekani nchini Ankara na Mjumbe Maalum wa Syria, amekuwa akiishi jijini Damascus. Kufuatia kufunguliwa tena kwa makaazi ya ubalozi wa Marekani jijini Damascus mwezi Mei, kumekuwa na mtiririko wa mikutano ya mara kwa mara na upatanishi wa ajabu kati ya Washington na Damascus. Kuanzia kamanda wa CENTCOM hadi maafisa wengi wa kijeshi, kuanzia wanadiplomasia wa ngazi ya chini na ya juu hadi wawakilishi wa makampuni ya mafuta na uwekezaji—kila mkoloni anazuru Damascus chini ya mwongozo wa Tom Barrack ili kuhakikisha utiifu kamili wa Syria kwa mipango miovu ya Amerika. Kila ziara na mkutano huongeza utiifu wa utawala wa Sharaa kwa Marekani, hukaza kamba iliyowekwa shingoni mwa Syria, na kuongeza viungo vipya kwenye mnyororo wa usaliti wa mapinduzi ya Kiislamu.
Trump mwenye kiburi akituma barua akimtaja Sharaa kwa jina, akielezea kuridhika kwake, na kumsifu—na hivyo kumtukana hadharani—pia ni matokeo ya utiifu huu wa upofu. Pia inafahamika kwamba ujumbe wa Trump ulitumwa baada ya ziara ya Ahmed Sharaa katika Ikulu ya White House na kwamba barua hiyo ilijumuisha picha iliyopigwa katika Afisi ya Oval. Kwani baada ya mkutano huo, utawala wa Damascus ulifanya kitendo kizito kwa kukubali kujiunga na muungano unaoitwa wa kupambana na ISIS—ambao kwa kweli ulikuwa Muungano wa Makruseda ulioanzishwa kupigana vita dhidi ya itikadi ya Kiislamu na fikra ya kutawala kwa Uislamu.
Matokeo ya kwanza ya ushiriki huu, ambao hauwezi kuelezewa ima kisheria (Shar'i) au kisiasa, bila shaka utakuwa ni kulenga—mmoja baada ya mwengine— wale wanaotabanni Uislamu kama mfumo kamili wa maisha na utawala, iwe ni Wasyria au Muhajir. Hakika, operesheni kama hizo tayari zinaendelea. Baada yake, itawawajibisha wale wote watakaokaa kimya dhidi ya udhalilifu huu na kupuuza majanga itakayoleta!
Usaliti huu ni mkubwa sana kiasi kwamba Marekani hapo awali ilikuwa imefanya majaribio mawili makubwa ya kutekeleza ushirikiano ambao utawala wa Damascus sasa umeukubali rasmi: “utaratibu wa uendeshaji” mwaka wa 2012 na miradi ya “kufunza na kuhami” mwaka wa 2014. Lakini FSA na makundi mengine ya upinzani yalikataa kupigana na Waislamu na kukataa kufanya kazi na Marekani, kwa hivyo mradi huo ulifeli. Wakati huo, mapinduzi ya Syria yalikuwa yakisonga mbele kwa imani kamili kwa Mwenyezi Mungu na uaminifu kwa kanuni za Kiislamu—kabla ya nchi kama Uturuki, Saudi Arabia, na Qatar kuingia kupitia kulia, kuyakamata mapinduzi huko Idlib, na kuyanasa katika mpango wa “utawala wa ndani”.
Sasa turudi kwenye barua ambayo gavana wa kikoloni wa Trump Tom Barrack alimpa Ahmed Şharaa: katika picha hii iliyo na sentensi moja na picha moja, kuna maelfu ya jumbe kwa wale wanaoweza kuelewa. Wa kwanza unaokuja akilini ni huu: Aibu ni sehemu ya Iman; mtu anayepoteza hisia zake za aibu anaweza kutoa taswira yoyote anayotaka na kufanya chochote anachotaka. Kwa upande mwengine, ikiwa Marekani inawekeza kiasi hiki kwa Ahmed Sharaa, mtu anajiuliza ni kwa muda gani mifupa ya mashahidi wa Bilad al-Sham itaendelea kuuma. Kwani miongoni mwa majukumu mapya yaliyolazimishwa kwa Sharaa na sifa za Trump ni pamoja na kukabidhiwa kwa eneo la kusini-magharibi mwa Syria kwa udhibiti wa umbile la Kiyahudi, kujiunga na Makubaliano ya Abraham, kuanzishwa kwa kambi za Marekani jijini Damascus, na utekelezaji wa makubaliano mengi muhimu kuhusu utafutaji wa mafuta wa makampuni ya Marekani kando ya pwani ya magharibi ya Syria. Ikilinganishwa na dhambi na hatari ya baadaye inayobebwa na makubaliano haya, kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Syria chini ya Sheria ya Kaisari si muhimu.
Na sasa, huku tukiwahisabu wahusika, hebu tuulize swali halisi: Baada ya maadhimisho ya kwanza ya siku ya ukombozi mnamo 8 Disemba, ni nini kilichobaki mikononi mwa Syria? Mapinduzi yaliyozikwa ardhini; heshima iliyopotea; Umma ambao ni imara lakini sasa umefungwa minyororo na kudhalilishwa... Na haya yote kwa badali ya nini? Kwa kile kinachoitwa utulivu na maendeleo yaliyoahidiwa na mkoloni, Kafiri Marekani? Kwa Jamhuri ya Kiarabu yenye mgawanyiko na uharibifu ambayo imependelewa zaidi ya mradi wa Khilafah ya Kiislamu—mwavuli wa umoja na heshima kwa umma, ambao watu wa Syria walilipa gharama kubwa? Kwa ajili ya kupatanisha na kuhalalisha mahusiano na umbile la Kiyahudi kwa gharama ya uharibifu wa Gaza? Kwa ajili ya kutoa “ng'ombe dume wa manjano” ili “ng'ombe dume mweusi” aweze kuishi muda mrefu zaidi?
Historia ya mbali na ya hivi karibuni imejaa mifano ya wale waliotafuta madaraka, heshima, na hadhi mahali popote isipokuwa katika Uislamu—na ambao waliishia katika hasara katika ulimwengu huu na ujao. Kwa hivyo, je, Ahmed Sharaa atazingatia na kurudi kwenye misingi ya mapinduzi ya Syria? Je, atatambua kwamba yeye si kiongozi wa kikundi tena bali anawajibika kwa watu wote wa Syria na ardhi zake zote? Je, atatafakari na kutenda tena kwa kutangaza kwamba mapinduzi ni fikra ambayo kamwe haiishi; kwamba mapambano halisi huanza baada ya kupata madaraka; na kwamba anapomtegemea Mwenyezi Mungu na umma, hakuna kikwazo kisichoshindika? Au atachagua kuishi chini ya udhibiti wa Marekani na Mayahudi, ndani ya tundu la dola ya kitaifa ya kisekula, kama mateka miongoni mwa mateka—akibeba mzigo wa watu wa Syria, Gaza inayokandamizwa, na umma mzima, akichagua udhalilifu na hasara?
[مَثَلُ الَّذِينَ اتَّخَذُوا مِنْ دُونِ اللَّهِ أَوْلِيَاءَ كَمَثَلِ الْعَنكَبُوتِ اتَّخَذَتْ بَيْتًا وَإِنَّ أَوْهَنَ الْبُيُوتِ لَبَيْتُ الْعَنْكَبُوتِ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ]
“Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua.” [Surah Al-Ankabut: 41]
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Muhammed Emin Yıldırım



