Alhamisi, 05 Rabi' al-awwal 1447 | 2025/08/28
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Waafghani Baina ya Nyundo ya Siasa za Pakistan na Kinoo cha Agenda ya Kikanda
(Imetafsiriwa)

Gazeti la Al-Rayah – Toleo 562 - 27/08/2025 M

Na Bilal Al Muhajir – Wilayah Pakistan

Tangu mwaka wa 2023, serikali ya Pakistan imezidisha uhamishaji wa wakimbizi wa Afghanistan, hatua inayolenga kuishinikiza serikali ya mpito ya Afghanistan inayoongozwa na Taliban jijini Kabul kuwasilisha kikamilifu matakwa ya Amerika. Mawimbi ya Waafghani kuhamishwa kwenda Pakistan yana mizizi ya kihistoria tangu Jihad dhidi ya Muungano wa Kisovieti katika miaka ya 1980, vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyofuata, na uvamizi wa Marekani na kuikalia kijeshi Afghanistan kuanzia 2001 hadi 2021. Pakistan kihistoria imetoa kina cha kimkakati kwa Waislamu wa Afghanistan, shukran kwa mafungamano ya karibu ya kabila yanayovuka Mstari wa Durand.

Kulingana na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), idadi ya wakimbizi wa Afghanistan nchini Pakistan ilifikia kilele mwaka 2002 na kufikia takriban milioni tatu, ambapo takriban milioni 1.35 walisajiliwa rasmi. Katika miongo miwili iliyopita, Pakistan imeendelea kuwafukuza wakimbizi wa Afghanistan kwa viwango tofauti. Kundi la Migogoro ya Kimataifa linakadiria kuwa wakimbizi wa Afghanistan nchini Pakistan wako katika makundi matatu:

1- Wamiliki wa kadi za Uthibitisho wa Usajili (PoR) zinazotolewa na UNHCR.

2- Wamiliki wa Kadi za Raia wa Afghanistan (ACC) zinazotolewa na serikali ya Pakistan.

3- Idadi kubwa wasio na hati zozote rasmi.

Sera ya Pakistan kuhusu wakimbizi wa Afghanistan imepitia awamu tatu kuu:

Awamu ya 1: Jihad ya Afghanistan dhidi ya Muungano wa Kisovieti (miaka ya 1980 na kuendelea): Wakati wa uvamizi wa Usovieti wa Afghanistan, Pakistan ilifungua mipaka yake kwa wakimbizi wa Afghanistan, kulingana na mkakati wa Marekani ambao ulitaka kugeuza Afghanistan kuwa “Vietnam ya Muungano wa Kisovyeti.” Wakimbizi hawa walitumiwa kuunda na kutoa mafunzo kwa vitengo vya wapiganaji vinavyojulikana kama “Mujahidina wa Afghanistan” kutekeleza operesheni dhidi ya vikosi vya Usovieti. Mpaka ulibaki wazi hata baada ya kujiondoa kwa Usovieti mnamo 1989, na udhibiti mdogo kuwekwa ili kuepusha mzozo wowote na Afghanistan.

Awamu ya Pili: Baada ya Septemba 11, 2001: Kwa kuwasili kwa Rais Pervez Musharraf, mtu anayeunga mkono na Washington, sera ya Pakistan dhidi ya Waafghani ilibadilika sana. Wapiganaji waliowahi kusherehekewa sasa waliitwa “magaidi.” Pakistan ilitakiwa kuunga mkono uvamizi wa Marekani dhidi ya Afghanistan na kuzuia makabila ya Pashtun kuwaunga mkono Taliban. Mpaka ulifungwa kwa kiasi, kampeni za vyombo vya habari zilianza kuwahusisha wakimbizi na uhalifu na madawa ya kulevya, na marekebisho ya kisheria yalianzishwa ambayo yalibatilisha hadhi maalum ya maeneo ya makabila (FATA) na kuwaingiza katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa. Malengo yalikuwa mawili: kuwaandama viongozi wa mujahidina wanaojificha miongoni mwa wakimbizi, na kuunda mgawanyiko wa kudumu baina ya Waislamu wa pande zote mbili za mpaka, ili kukwamisha mradi wowote wa umoja wa Kiislamu, hasa chini ya mwavuli wa Khilafah, ambao jina lake lenyewe linatishia Magharibi na washirika wake.

Awamu ya Tatu: Baada ya Kujiondoa kwa Marekani (2021): Kujiondoa kwa Marekani mnamo Agosti 2021 kulisababisha kuongezeka kwa mvutano kati ya makabila ya Wapashtun katika pande zote za mpaka, ambao walishikilia Pakistan kuhusika na uharibifu mkubwa uliotekelezwa katika maeneo yao wakati wa operesheni za kijeshi tangu 2002. Huku Taliban ya Pakistan ikianzisha tena mashambulizi dhidi ya Jeshi la Pakistan kujibu shinikizo la kijeshi na kutelekezwa kwa maeneo yao, mamlaka zilikazanisha hatua za kiusalama, na kugeuza suala la wakimbizi kuwa chombo cha shinikizo kwa Taliban ya Afghanistan, na kuzidisha mgawanyiko kati ya watu wa pande hizo mbili.

Sera ya Sasa: ​​Awamu ya kwanza ya mpango mpya wa uhamishaji ilianza Novemba 2023, ikilenga takriban Waafghani milioni 1.3 wasio na hati. Kufikia Februari 2025, Pakistan ilikuwa imewafukuza kwa lazima zaidi ya 800,000 kati yao. Mnamo Januari 2025, Waafghani walioishi Islamabad na Rawalpindi walilazimishwa kuondoka kufikia Machi 31, chini ya “cheti cha kutopinga” (NOC). Mnamo Machi, Wizara ya Mambo ya Ndani ilibatilisha kadi zao za ukaazi (ACCs) na kuamuru wamiliki wao kuondoka mwishoni mwa mwezi. Pia iliacha kujadidisha kadi za Uthibitisho wa Usajili (PoR) baada ya Juni 30, na kutishia kufukuzwa kwa wakimbizi wengine milioni 1.6. Kwa mujibu wa shirika la Amnesty International, Pakistan iliwafukuza kwa lazima angalau Waafghani 844,499 kati ya Novemba 2023 na Februari 2025, na kuongeza muda wa makataa wa kuwafurusha waliosalia hadi Septemba 1, 2025.

Kwa hivyo, dola ya Pakistan, ambayo hapo awali ilianzishwa kwa msingi wa kuwaunganisha Waislamu katika Bara dogo la India na kuwa umbo lenye Waislamu wengi, hivi leo inawafukuza Waislamu waliokimbia maafa ya vita vilivyoanzishwa na Muungano wa Kisovieti, na kisha Marekani, dhidi ya Afghanistan na watu wake, na kupuuza ukweli kwamba Waislamu ni Umma mmoja, na hakuna tofauti kati ya Muafghani na Mpakistani, au Muarabu na asiyekuwa Muarabu, isipokuwa kwa uchaMungu, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema, يا أيها الناس، ألا إن ربكم واحد، وإن أباكم واحد، ألا لا فضل لعربي على أعجمي، ولا لعجمي على عربي، ولا لأحمر على أسود، ولا لأسود على أحمر إلا بالتقوى   “Enyi watu, Mola wenu ni mmoja, na baba yenu ni mmoja, jueni hakuna ubora wa Muarabu juu ya asiyekuwa Muarabu, wala asiyekuwa Muarabu juu ya Muarabu, wala mwekundu juu ya mweusi, wala mweusi juu ya mwekundu, isipokuwa katika uchamungu.” (Imepokewa na Ahmad)

Serikali ya Qatar, iliyowekwa na ukoloni wa Kimagharibi, ipo ili kuzusha migogoro ya mipaka ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu na kupoteza rasilimali zinazolinda mipaka ya kitaifa badala ya kuzielekeza kwenye Jihad. Kwa mfano, Pakistan ilitumia dolari milioni 500 kujenga uzio wa mpaka kando ya Laini ya Durand, badala ya kuziwekeza katika kuwapa mafunzo wapiganaji ili kuikomboa Kashmir Inayokaliwa kimabavu. Zaidi ya hayo, kukazwa kwa sera za mpaka na wakimbizi kumeanza kupandikiza chuki dhidi ya Pakistan na watu wake nchini Afghanistan, na hivyo kuathiri biashara kati ya nchi hizo mbili na Asia ya Kati. Kwa hivyo, mizozo inayotokana na kufukuzwa kwa lazima hutumikia maslahi ya maadui wa Ummah, hasa Marekani na India, na kuzuia ukaribu wowote au umoja kati ya Pakistan na Afghanistan.

Hatimaye, ni lazima ikumbukwe kwamba fahamu ya “mkimbizi” haipo katika Uislamu. Waislamu ni Ummah mmoja, na Muislamu huhama kati ya maeneo ya Ulimwengu wa Kiislamu, mithili ya mtu kuhama baina ya vyumba vya nyumba moja. Usalama na uthabiti haupatikani kwa kuugawanya Ummah katika dola ndogo ndogo zilizotenganishwa na sera ya kikoloni, bali kupitia Dini ya Uislamu na kushikamana na Shariah ya Kiislamu. Kukosekana kwa dola inayounganisha kimfumo ya kisiasa ndiyo sababu kuu ya machafuko yanayoikumba Pakistan na nchi nyingine za Kiislamu hivi sasa. Hivyo, kufanya kazi ya kusimamisha Khilafah Rashida kwa Njia ya Utume, ni hitajio la usalama na pia ni faradhi wa Shariah.

[إِنَّ هَذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ]

“Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.” [Al-Anbiya:92]

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu